DC-KIBAHA AZINDUA KANZIDATA YA MACHINGA MKOA WA PWANI
Na Byarugaba Innocent, Kibaha
Mkuu wa Wilaya Kibaha Mhe. Nickson Simon John, leo Alhamisi tarehe 16 Novemba, 2023 amezindua kanzidata ya Wafanyabiashara wadogo 'Machinga'katika Mkoa wa Pwani ili watambulike rasmi na Serikali na kuunganishwa na taasisi za kifedha.
Mhe.Nickson amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan inatambua mchango mkubwa wa wafanyabiashara wadogo nchini ndio maana inawekeza kwenye kuweka Mazingira wezeshi ikiwemo kujenga Ofisi maalum ili waweze kupata sehemu ya uongozi na kujadili mambo yao.
Mwenyekiti wa wafanyabiashara wadogo Mkoa wa Pwani Filemon Maliga ameeleza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ametoa kiasi cha Bilioni 45 kwa ajili ya Mikopo yenye riba nafuu yenye riba asilimia 7 kwa wafanyabiashara wadogo na kwamba fedha hizo zitatolewa kupitia Benki za CRDB, NMB na Benki ya Posta.
Aidha, Maliga ametoa wito kwa wafanyabiashara wadogo wote 57,000 waliopo Mkoa wa Pwani kujisajili kikamilifu ili waweze kunufaika kwani Serikali na taasisi za kifedha hufanyakazi kwa takwimu sahihi.
"Mhe Rais ana ndoto ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wadogo wote Wanaendelea na kufikia Uchumi wa juu" ameongeza Maliga